Parish Details
HISTORIA YA PAROKIA YA
MT. THERESIA WA MTOTO YESU -
KAHAMA
Kigango cha Mt. Theresia
wa Mtoto Yesu – Kahama, kilianzishwa mnamo mwaka 1974, Wakati huo walikuwa
wanasali nyumbani kwa Judith Kapesa, ambae alihudumu kama katekista kwa wakati
huo. Mwaka 1983, walihamia katika maeneo ya shule ya msingi Kahama, wakiwa
chini ya katekista TRYPHONE KABABASHE NG’HOLONGO, wakiwa chini ya Parokia ya Mt.
JUSTINE – BUJORA. Baada ya kufariki katekista TRYPHONE, Waliendelea kusali
wakiwa na katekista CLEMENT LUMU MAYALA.
Mnamo mwaka 1985
walianza ujenzi wa Kanisa katika eneo walilopewa na serikali ya kijiji chini ya
uongozi wa Andrea Mang’weng’ula (mwenyekiti wa kijiji) na Zabron Kalimbia
(kamati ya ugawaji ardhi), wakati huo walikuwa chini ya katekista Venance
Makelele. Walianza ujenzi wa kanisa la tope na kuezeka kwa nyasi kwa kutumia
nguvu za waumini. Na mwaka 1994 walipata ufadhili wa mabati hamsini (50) kutoka kwa Padre KALORI wa parokia ya
Kawekamo, na wakati huo walikuwa chini ya usimamizi wa katekista Joseph Ludaila
Nyanda.
Mwaka 2005 kigango cha
Mt. Theresia wa Mtoto Yesu kilikabidhiwa chini ya usimamizi wa parokia ya Mt.
Josephina Bakhita – Igoma chini ya usimamizi wa Padre ANDREA. Wakati huo
kigango kilikuwa na jumuiya nne (4), ambazo ni jumuiya MT. THERESIA, VERONICA,
MARIA NA YOSEPH, na wakati huo kigango cha Kahama kilitumika kama senta ya
vigango vitatu ambavyo ni Igogwe, Nyamadoke na Kahama. Mwaka 2014 jumuiya ya
Mt. Maria iligawanywa na kupata jumuiya ya Mt. Petro ambayo baadae
ilianzisha kigango cha Isela.
Tarehe 01/01/2018,
kigango kiliwekwa chini ya usimamizi wa parokia ya Bikira Maria Mama wa Mungu –
Buswelu, kikiwa na jumuiya ndogo ndogo kumi na saba (17). Wakati huo kigango
kilikuwa chini ya katekista Christopher Swalala ambaye kwa sasa ni
marehemu. Tarehe 26/09/2020 kigango cha Mt. Theresia wa Mtoto Yesu – Kahama
kilitangazwa kuwa Parokia Teule na Mhashamu Baba Askofu Mkuu Renatus Leonard
Nkwande, chini ya usimamizi wa Padre Faustine Yohane Bagwa hadi leo tarehe
29/10/2022, Parokia Teule Kahama ina vigango vitatu ambavyo ni kigango cha
Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu – Kahama chenye jumuiya ishirini (20) na mitaa
tisa (9), kigango cha Mtakatifu Petro Mtume- Ilalila chenye jumuiya sita (6) na
kigango cha Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu – Igogwe chenye jumuiya tano (5).
Hivyo Parokia Teule ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu – Kahama ina jumla ya
vigango vitatu (3), mitaa tisa (9) na jumuiya thelathini na moja (31).