Parish Details
HISTORIA FUPI YA
PAROKIA YA
MT. PETRO MTUME - NG’HUNGUMALWA
Kigango cha Ng’hungumalwa kilianzishwa mnamo mwaka 1974
kikitokea Mwamhaya ambako waamini wa Nyanhiga na Ng’hungumalwa walikuwa
wanasali Mwamhaya. Katekista wa Mwamhaya kwa wakati ule alikuwa ni Yakobo
Mviji. Baada ya kuanzishwa kigango cha Ng’hungumalwa, Katekista wa kwanza
alikwa Bonaventura Fugongali (Marehemu).
Waumini walianza kusali katika eneo ambalo hapakuwa na
jengo lolote, walianzia palipo na machinjio kwa sasa. Mwaka 1975 waliomba
kiwanja katika serikali ya Kijiji, walipewa eneo la ekari 1.5 ambapo
waliendelea kusali hadi mwaka 1988 ambapo kiwanja kilikatwa na grid ya Taifa
mwaka 1989, waliomba tena eneo jingine ambalo wanalo mpaka sasa. Baada ya
kupewa na serikali ya Kijiji kiasi cha ekari 33.
Makatekista wa kwanza ni:- Bonaventura Fugongali, Leontina
Shigu, Gaspar Luhonola, Berali Mbilingi, Didas Budila, Lucas Gunanangila,
Deogratias Bugode, Francis Tissian, Mariana Kundi, Clement Shilinde hadi sasa.
Mwaka 1996 ulitokea mgogoro katika eneo la kanisa dhidi ya
Mwenyekiti wa Kijiji aliyehodhi ardhi ya Kanisa kwa mamlaka aliyokuwa nayo,
kesi hiyo ilidumu miaka 3 na kumalizika mwaka 1998 ndipo Kanisa liliposhinda
kesi mahakamani.
Shukrani kwa Deogratias Kibungi
Mwenyekiti wa Kigango wakati ule (marehemu), aliyesimamia kesi hadi haki ikapatikana.
Pia kwa Bonaventura Fugongali
Katekista wakati ule (Marehemu) aliyetoa Ushahidi mahakamani. Pia tunamshukuru
Clement Shilinde katibu wa Kigango wakati ule aliyetoa Ushahidi Mahakamani hadi
haki ikapatikana. Pia Mzee Sabini Ngeleja alikuwa mshauri katika kesi hiyo.
Kigango cha
Ng’hungumalwa kilikuwa sehemu ya Parokia ya Mt. Anna Mwabagole ikiongozwa na
Padre Karoli Zimameni (Paroko) na Padre Ferdinand Baremare (Paroko msaidizi )
wakitokea katika shirika la White Fathers.
Katika kukua na
kuimarika kiimani, kigango cha Ng’hungumalwa kilirasimishwa na kupandishwa
hadhi na kuwa Parokia Teule mnamo tarehe 04/08/2016 na Mhashamu Askofu Mkuu
Juda Thadeus Ruwa’ichi aliyekuwa askofu wa Jimbo Kuu la Mwanza.
MAPADRE WALIOWAHI
KUHUDUMU PAROKIA TEULE HII YA NG’HUNGUMALWA
Katika historia,
Kanisa kwanza linawashukuru mapadre wote waliowahi kutoa huduma za kiroho na
kuchangia kukuza na kuimarisha imani kwa waamini hapa Ng’hungumalwa; Padre
Karoli Zimameni, Pd. Ferdinand Baremare, Pd. Francis Bahebe, Pd. John Buluma,
Pd. Justine Mabula, Pd. Bruno Mahenda, Pd. Pius bilulu, Pd. Mathayo Bujiku, Pd.
Claud Mpuya, Pd. Robert Kitambo, Pd. Francis Mtema, Pd. Maximilian Buluma, Pd.
Andrea Msonge, Pd. Zacharia Makoye, Pd. Casmir Bulugu, Pd. Christopher Baluhya,
Pd. Mikael (SMA), Pd. Thomas (SMA), Pd. John Krikoin (SMA), Pd. Misheli (SMA),
Pd. Anthon Lachaga (SMA), Pd. Deogratias Malekanya.
Hali kadhalika tunapenda kutoa
shukrani zetu za dhati kwa mapadri wafuatao kwa kuendelea kutoa huduma na
kushirikiana na Parokia kwa ujumla, kwani wamekuwa chachu ya kuimarika kiroho
na maendeleo ya kanisa kwa ujumla yaani:- Pd. Costantine Sendama (Paroko
Nyabulogoya), Pd. Theophil Kumalija (Parokia ya Sahwa), Pd. Pd. John Nkwabi (
Paroko Tarazo), Pd. George Nzungu (Paroko Nyamhongolo), Pd. John Kasembo
(Paroko Kitumba), Pd.Gerald Kabomo (Kawekamo na Ofisi ya Askofu Mkuu), Pd.
William Ndonhe (Nyegezi Seminari).
Hali kadhalika, tunamshukuru padre Raso Litaka wa
Jimbo la Mahenge anayefanya utume katika Seminari Kuu ya Mt. Paul Kipalapala
Jimbo Kuu la Tabora, kwa majitoleo na muda wake kwa ajili ya kutoa huduma
katika parokia yetu inayozinduliwa leo.
Pia tunamshukuru padre Charles Masaga (Dokta Maua)
toka parokia ya Nyabulogoya kwa kuwa bega kwa bega na waumini hadi leo hii
tumefikia kuzinduliwa. Amehudumu hapa na kushauri mambo mengi.
Wote hawa wamekuwa msaada mkubwa sana katika kutoa huduma
za kiroho katika parokia hii Teule; Ahsanteni sana Mungu awape afya njema.
Pia kwa namna ya pekee tunamshukuru
sana Baba Paroko wetu Pd. Fabian Mhoja (Shigulu shabuki) anayehudumia
mpaka sasa kwa kutuongoza vyema na kutoa huduma za kiroho katika maeneo yote ya
vigango vyetu. Baba Paroko wetu amekuwa mtumishi na chachu ya maendeleo ya
Parokia Teule hii kwa kuhamasisha na kufundisha imani thabiti ya kanisa na
uchungaji mwema hasa kwetu sisi. Pia tunamshukuru kwa uhamasishaji wa maendeleo
ya kanisa hasa kwa kuhamasisha ujenzi wa nyumba ya mapadre vigango na kanisa
kwa ujumla; tunasema asante sana Mungu akujalie afya njema na utume mzuri
uendelee kutuhudumia.
VIONGOZI HALMASHAURI WALEI
Tunawashukuru sana viongozi waanzilishi wa kigango
waliotumika kuasisi na waanzilishi kama ifuatavyo:-
Mzee Aloyce Petro (Marehemu), Mzee Deogratias Kibungi
(Marehemu), Mzee Clement Kalemani (Marehemu), Mzee Stephen Yamala, Daniel,
Magdalena Joseph (Marehemu), Marietha Petro (Marehemu), Anastazia na Temela.
Hawa walifanya utume wao vizuri na mwenyezi Mungu awarehemu wote waliotangulia
mbele za haki na wale waliopo hai Mungu awazidishie kwa kutumika na utume wenu
Baraka zake zikae nanyi na familia zenu.
VIONGOZI WALIOPO
KWA SASA MPAKA LEO
Viongozi hawa
tunawaombea waendelee na utume wao kwa kumtanguliza Mungu zaidi maana
wamechaguliwa na Mungu na tunawashukuru kwa kuendelea kutumikia kanisa hadi leo
tunapozinduliwa kuwa Parokia rasmi. Shukrani nyingi kwa hawa
wafuatao; Deogratias Masanja (Mwenyekiti), Deogratias Fabian (M/Mwenyekiti),
Zakayo Togoi (Katibu), Leonard Justine (M/Katibu) Thelezia Andrea (Mhasibu) na
Richard B. Stephen (Katibu Mtendaji).
MAKATEKISTA
Walezi wetu wa kiroho makatekista wanaohudumu katika
parokia Teule hii mpaka sasa tunao Makatekista wafuatao:- Clement Shilinde
(Mwenyekiti), Stephen Henerco (M/Mwenyekiti), F. Bunane (Katibu), Mariana
Shilinde
(Mhasibu) Gerald Gasembe (Mratibu), George, Yulitha
Shilangi, Francis Tisian, Justine Philipo, Raphael Luhunga, Felister John,
Razalo Masele, Maria Makaji, Costantine Busongo, Paulo Lugolola, Sylivester na
Aloyse John (Katibu Msaidizi).
MAKATEKISTA WAANZILISHI
Bonaventura Fugongali (Marehemu), Leonstina Shigu
(Marehemu), Gaspary Luhonola (Marehemu), Didas Bundila (Marehemu).
MAKATEKISTA WASTAAFU
Paschal, Deogratias, Elias Masheku.
JUMUIYA
Wakati Kigango kinaanzishwa kilikuwa na Jumuiya ndogondogo
za Kikristu tatu (3) tu ambazo ni Moyo Mtakatifu wa Yesu, Rozali
Takatifu na Utatu Mtakatifu. Pia kigango kilianza na familia za
Kikristu 52 tu na sasa hivi tunazinduliwa tukiwa na familia za Kikristu 1200 na
Jumuiya za Kikristu 75. Tunashukuru Mungu kwa Injili kutufikia na kuamsha Imani
na Mshikamano katika kumtangaza Kristo kama ilivyo Kauli mbiu yetu.
SHUKRANI
Tunakushukuru sana Mhashamu Askofu Mkuu Renatus Nkwande kwa
kuridhia leo hii katika historia ya kanisa letu kuipandisha hadhi na
kuzinduliwa kuwa Parokia kamili. Leo ni siku pekee sana kwa wanaparokia hii,
maana ni safari kubwa na ndefu mpaka kufika leo na kusimikwa Parokia. Tunasema
tena asante sana na Mungu akupe afya njema katika utume wako wa kila siku
katika Jimbo letu.
Tunamshukuru kwa namna ya pekee Hayati
Askofu Mkuu Anthony Petrus Mayala kwa kutuhimiza kununua maeneo makubwa kwa
ajili ya makanisa.
Tunatoa shukrani za pekee kwa Mikael Majige kwa kununua
eneo la Kanisa ambalo tunalitumia, yeye aliamua kutoa fidia kwa watu ambao
walikuwa wanalitumia eneo hili. Yeye hakutaka kuwepo na mgogoro mwingine. Mwaka
1999, tulianzisha ujenzi wa kanisa, marehemu Mikael Majige alijitolea kujenga
kanisa kwa majitoleo mengi sana vikiwemo saruji, fedha za kulipa mafundi pamoja
na usafiri.
Tunamshukuru tena marehemu Mikael Majige, aliyethubutu
kufanya majitoleo ya hali na mali kwa kanisa letu, kwa kununua ardhi ya Ekari
32 na kuitoa kwa kanisa hili. Pamoja
na fedha za kuanzisha ujenzi wa kanisa tunaloliona leo. Kwa namna ya pekee
alifanya tendo la pekee sana, Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa amani - Amina.
Shukrani nyingi
zimwendee Padri Casmir Bulugu aliyeanzisha Msingi wa Kanisa tunaloliona leo.
Pia alianzisha jengo la chekechea, tunasema ahsante sana. Tunatoa shukrani za
dhati kwa WATAWA nyumba ya Mwahoba (Shirika la mabradha wa Moyo Mtakatifu wa
Yesu) likiongozwa na kaimu Br. Simeon Sahani.
MWISHO
Tunawashukuru kwa
moyo wa dhati walezi wetu Parokia ya Mt. Anna Mwabagole, wamekuwa wazazi bora
na hakika wametulea katika malezi mema mpaka leo tunazinduliwa na kuwa Parokia
rasmi, hii yote ni kwa malezi mazuri waliyotupatia ya upendo, uvumilivu na
majitoleo katika misingi ya kiimani. Wametusaidia katika mengi, tunasema
asanteni sana familia yote ya Parokia ya Mwabagole.