Parokia ya Kung'ara Bwana Wetu Yesu Kristu - Mabatini ni miongoni mwa parokia zilizomo ndani ya udekano wa Bugando, Jimbo Kuu la Mwanza CHIMBUKO Parokia ya Mabatini ilikuwa miongoni mwa vigango saba vilivyokuwa chini ya Parokia ya Bugando. Mnamo mwaka 1964, kundi la wakristu walianza kusali nyumbani kwa mzee Petro Bundala chini ya uongozi wa Charles Mapembe. Mwaka 1969 waumini hawa waliomba na kupata eneo toka kwa mwenyeji Yacob ambapo walijenga kigango cha matope chini ya Askofu Renatus Butibubage na Paroko wa Parokia ya Bugando Padre Yakobo Hoosdergt. Baadaye mwaka 1994 waumini walijenga kigango kwa kutumia nguvu zao wenyewe na misaada kutoka kwa wahisani mbalimbali. Mwaka huo huo 1994, uongozi wa Kigango uliandika barua kwa Paroko Padre Michael Mayela kuomba kupatiwa Misa Takatifu kigangoni. Ombi hilo lilikubaliwa na misa ya kwanza iliadhimishwa katika sikukuu ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristu [Ekaristi Takatifu] mwezi June, 1994. Padre Jimmy Eble ambaye ni Paroko wa kwanza na muanzilishi wa Parokia hii, katika miaka ya 2000 alikuwa akifanya kazi kama mwalimu wa ushauri nasaha katika hospitali ya Bugando. Alikuwa akiombwa na Paroko wa Parokia ya Bugando wakati ule Padre Tryphone Magafu kumsaidia kutoa huduma ya Misa Takatifu Jumapili na sikukuu za kanisa katika vigango vya parokia ya Bugando, ambapo alipangiwa kutoa huduma Mabatini. Mnamo mwaka 2001 mwezi Januari, Padre Jimmy Eble wa shirika la wamisionari wa Maryknoll alipangiwa rasmi na Paroko wa Bugando Padre Tryphone Magafu kuwa mlezi wa Kigango hiki cha Mabatini kwa matumaini ya kuwa Parokia Teule baadaye. Padre Jimmy Eble akisaidiana na Padre Donati waliongoza Kigango hiki kwa kufuata mwongozo wa Jimbo Kuu la Mwanza kuhusu huduma za sakramenti, uongozi na hatua za kuwa Parokia. Viongozi wa kigango chini ya mwenyekiti wakati ule Renatus Manyama waliongea na Padre Jimmy na kumdokeza kuhusu nia na tamaa ya kufanya kigango cha Mabatini kuwa Parokia na kwa namna ya pekee kumwomba Padre Jimmy kuja kuanzisha Parokia hii. Mazungumzo hayo Padre Jimmy aliyaweka moyoni na baada ya kumaliza mkataba wake katika hospitali ya Bugando, aliyatafakari mazungumzo hayo na kufikia uamuzi wa kukubali kuja Mabatini kuanzisha Parokia. Padre Jimmy alifanya mazungumzo na Baba Askofu Mkuu Mhashamu Anthony Petro Mayala [Mungu aipumzishe Roho yake mahali pa Amani mbinguni.] pamoja na wakuu wa shirika la Maryknoll kwa pamoja waliafiki wazo hilo na ndipo Padre Jimmy alianza kutoa huduma na kufanya maandalizi ya Parokia. Padre Jimmy alianza kwa kuzitembelea jumuiya zote akitoa semina na kukusanya maoni ya wanajumuiya kuhusu kuanzisha Parokia. Baada ya kuridhishwa na moyo wa wanajumuiya wa Jumuiya zote kuwa wako tayari kushirikiana naye kuanzisha Parokia, alianza kufanya mazungumzo na maparoko wa Parokia zinazopakana na Mabatini kuhusu mipaka, wakati huo akiendelea kutoa semina kwa waamini kitendo ambacho alikiita “KUJENGA KANISA WATU.” Parokia hii ilikuwa ya kwanza kusimikwa baada ya Sinodi ya Jimbo Kuu la Mwanza yenye wito wa kuwa "Familia ya Mungu inayojali na kuwajibika." Katika mazungumzo na maparoko hao, Padre Tryphone Magafu - [Paroko wa Parokia ya Bugando] alikubali Kigango cha POLICE LINE MABATINI ambacho pia kilikuwa chini ya Parokia yake kiwe ndani ya Parokia mpya ya Mabatini. Baada ya makubaliano hayo, taarifa ya maandishi ilitolewa kwa Baba Askofu Mkuu Antony Petro Mayala, ambaye naye kwa kushauriwa na washauri wake aliafiki Mabatini iwe Parokia. Wakati wote huo Padre Jimmy alikuwa akishirikiana bega kwa bega na viongozi wa Halmashauri ya Walei ya Kigango ambao walikuwa hawa wafuatao:- o Mwenyekiti - Renatus Manyama o Makamu mwenyekiti - Pius Joseph o Katibu - Adam Kazungu o Katibu msaidizi - Joseph Mahega o Mtunza Hazina - Leonard Chama KUTANGAZWA PAROKIA TEULE: Mnamo mwaka 2002 Mhashamu Baba Askofu Mkuu Anthony Petro Mayala alikitangaza Kigango cha Mabatini kuwa Parokia Teule na kiliwekwa chini ya uangalizi wa Padre Jimmy Eble wa shirika la wamisionari wa Maryknoll. KUSIMIKWA PAROKIA Mnamo siku ya Jumapili tarehe 12/09/2004 Parokia teule ya Mabatini ilisimikwa rasmi kuwa Parokia na Mhashamu Baba Askofu Mkuu Anthony Petro Mayala, chini ya usimamizi wa Kristu -- kumbukumbu ya KUNG'ARA BWANA WETU YESU KRISTU, na alisisitiza kila mwaka, tarehe sita mwezi wa nane (6/8/) tuwe tunaiadhimisha siku hii kama Sikukuu ya Parokia yetu. Parokia ilikabidhiwa kwa Padre Jimmy Eble wa shirika la Maryknoll chini ya usimamizi wa mkuu wa shirika wakati huo Padre Thomas Tisconia na alisimikwa siku hiyo hiyo kuwa Paroko wa kwanza wa Parokia hii. Padre Donat Paroko msaidizi wakati huo, alikuwa wa kwanza kutoa ahadi ya utii kwa Paroko akifuatiwa na viongozi kamati tendaji Halmashauri ya Walei na baadaye viongozi wote wa Jumuiya. UONGOZI WA HALMASHAURI YA WALEI NGAZI YA PAROKIA: Baadaye ulifanyika uchaguzi wa viongozi wa Halmashauri ya Walei Parokia na kuchaguliwa wafuatao:- Mwenyekiti ¬ - Renatus Manyama Makamu mwenyekiti - Pius Joseph Katibu - Adam Kazungu Katibu msaidizi - Joseph Mahega Mtunza Hazina - Happy Douglas 2.0 SHUGHULI ZA UINJILISHAJI NA HUDUMA ZA KIROHO PAROKIANI: Parokia hii tangu ianzishwe imeendelea kufanya shughuli kubwa za uinjilishaji katika kujenga kanisa watu na majengo ya kanisa. Mnamo mwaka 2013 Padre Jimmy Eble alihama katika parokia yetu baada ya kuhudumu kwa muda wa miaka kumi (10) Baba Askofu Mkuu Jude Thaddeus Ruwa'ichi alimteua Padre Pamphilius Madata kuwa msimamizi wa Parokia au Paroko wa mpito - kama alivyopenda kumuita katika kipindi cha mpito, wakati shirika la Maryknoll linatafuta Padre mwingine wa kutoa huduma hapa. Baadae mwaka 2015 shirika la Maryknoll lilimteua Padre Lam Hua kuwa Paroko wa Parokia hii. Pia lilimteua Padre John Eyble kuwa Paroko msaidizi wa parokia hii ambaye kwa sasa ndiye Paroko wa Parokia ya Mabatini akisaidiwa na Padre John Siyumbu, MM. Huduma za uinjilishaji wanazitoa kwa pamoja kwa kushirikiana na Br. Loren pamoja na walei wa Maryknoll. Parokia yetu inao makatekista wanne ambao ni Godwin Michael, Elias Philipo, Emmanue Cosmas na Domina Yusto. Parokia yetu kwa sasa inaadhimisha misa mbili parokiani na misa moja katika kigango cha Mtakatifu Juda Thaddeus - Bethlehemu kila Jumapili na misa za "wiki" kila siku. Pia tuna maabudu ya Sakramenti Kuu ya Ekaristi Takatifu yaani [Benediksio] kila Alhamisi saa 11.00 jioni. HALI YA IMANI: Hali ya Imani imeendelea kuimarika ambapo waamini wengi zaidi wanaendelea kukua katika Imani na kubadili mwenendo wao wa maisha, ijapokuwa bado changamoto za uchanga wa Imani zinasumbua. Kiwango cha sadaka na majitoleo kinazidi kuongezeka ukilinganisha na mwanzo wakati parokia inasimikwa. Parokia inaendelea kutekeleza sera za Sinodi ya Mwanza pamoja na kushiriki na kuwajibika kikamilifu katika matukio na shughuli za kijimbo ikiwemo wiki ya ukarimu na shukrani, ujenzi wa Kanisa Kuu la Kiaskofu [Cathedral] na uimarishaji wa miito. HALI YA MIITO: Mpaka sasa parokia yetu imezaa mapadre wanne ambao ni Padre George Nzungu 2009, Padre Celestine Nyanda 2012, Padre Kelvin Mkama 2016 na Padre Enock R. Mutegeki 2022. MAENDELEO YA BAADAYE Baada ya kujenga kanisa watu, Padre Jimmy kwa kushirikiana na waamini pamoja na wafadhili mbalimbali ndani na nje ya Tanzania, tuliendelea kujenga majengo ya kanisa ambapo tumejenga kanisa kubwa lenye uwezo wa kubeba watu 1000 kwa wakati mmoja, nyumba ya mapadre, jengo la utawala, groto la Mama Bikra Maria na stoo. Pia serikali iliipatia parokia eneo katika kata ya Buzuruga ambapo tayari kumejengwa Kigango cha Mtakatifu Yuda Thaddeus. VYAMA VYA KITUME Parokia inavyo vyama vya kitume vya halaiki na hiari kama ifuatavyo:- o UWAKA o WAWATA o VIWAWA o Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu. o Legio Mariae o Karsmatiki katoliki o Kwaya - Kwaya ya Bikra Maria Malkia wa Amani, Kwaya ya Mtakatifu Martine o ,na Kwaya wa Mashahidi wa Uganda. o Wanawito o Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu MITAA: Parokia inayo mitaa mitano ambayo ni: o Mtaa wa Kanaani o Mtaa wa Msamaria Mwema o Mtaa wa Sayuni o Mtaa wa Butibubage o Mtaa wa Maryknool KIGANGO: Parokia inacho kigango kimoja ambacho ni Kigango cha Mtakatifu Juda Thaddeus- Bethlehemu. 3.0 MAFANIKIO: Katika kipindi chote hiki tumepata mafanikio mengi. Hata hivyo haya ni baadhi ya mengi ambayo yamepatikana hapa parokiani kwetu. o Parokia yetu imefanikiwa kujenga kanisa kubwa lenye uwezo wa kubeba watu 1000 kwa misa moja. o Tumefanikiwa kuhamisha wenyeji wanaokaa katika eneo la parokia. o Tumefanikiwa kupata mapadre wanne. o Tumefanikiwa kuanzisha kigango cha Mtakatifu Jude Thaddeus - Bethlehemu katika eneo la mtaa wa Nyambiti. CHANGAMOTO: Zipo changamoto mbalimbali zinazotukabili, zifuatazo ni baadhi o Bado tunakabiliwa na changamoto ya kubwa ambayo ni upatikanaji wa hati ya eneo la Parokia.