Mipaka Yake
Jimbo Kuu la Mwanza linaunganisha wilaya za Mwanza, Kwimba, Misungwi na sehemu ya magharibi ya wilaya ya Magu. Kufuatana na historia ya huko nyuma, Jimbo Kuu la Mwanza hapo awali lilikuwa ni sehemu ya eneo la mikoa ya maziwa makuu.
Chimbuko Lake
Kunako mwaka 1878 sehemu ya Buganda ilikuwa chini ya uongozi wa mapadre wa shirika la Wamisionari wa Afrika, Mwaka 1882 wamisionari walifukuzwa na Kabaka Mutesa, Mwaka 1883 wamisionari hao walifanya mapatano na Mtemi Kiganga ili waweze kuanzisha parokia ya Bukumbi. Kwa hiyo parokia hiyo ni ya kwanza katika eneo la mkoa wa sasa wa Mwanza. Sehemu ya Mwanza, Bukoba, Ngara, Biharamulo, Karagwe, Rwanda na Burundi ilijulikana kama viakarieti ya Nyanza chini ya uongozi wa Monsiniori Livinhac alipopewa uaskofu mwaka 1884.
Baadaye kunako mwaka 1890, Askofu Joseph Hirth kutoka Ujerumani aliongoza vikarieti ya Nyanza hadi 1912 wakati vikarieti hii ilipogawanyika kuwa vikarieti ya Rwanda na vikarieti ya Nyanza.
Vikarieti ya Nyanza iliyoundwa chini ya uongozi wa Monsiniori Joseph Sweens ilijumuisha majimbo yote ya sasa ya Jimbo Kuu la Mwanza isipokuwa Jimbo la Shinyanga. Monsiniori Sweens alikuwa akiishi Rubya mkoani Kagera aliendelea
2
kutawala hadi mwaka 1929 wakati vikarieti ya Nyanza ilipogawanyika kuwa Bukoba na Mwanza.
Vikarieti ya Mwanza iliongozwa na Askofu Anthony Oomen kuanzia mwaka 1929 hadi 1948. Ikumbukwe kuwa mwaka 1946, wilaya za Musoma, North-Mara na Maswa zilitenganishwa kutoka vikarieti ya Mwanza ili kuunda vikarieti mpya ya Musoma-Maswa. Wakati huo huo Shinyanga nayo iliondolewa kwenye Jimbo la Tabora na kuwa chini ya vikarieti ya Mwanza.
Askofu Joseph Blomjous aliyesimikwa kuwa Askofu mwaka 1946 alipewa madaraka ya kuongoza vikarieti ya Mwanza mnamo mwaka 1950 badala ya Askofu Oomen na pia kama mtawala wa vikarieti ya Musoma-Maswa.
Mwaka 1956 vikarieti ya Musoma-Maswa iligawanyika na kuwa majimbo ya Musoma na Maswa ambayo yalikabidhiwa kwa shirika la Maryknoll.
Tarehe 1 Mei Mwaka 1966 askofu Renatus Butibubage alianza kuongoza jimbo la Mwanza mpaka mwaka 1987 wakati alipostaafu.
Kuanzishwa kwa Jimbo Kuu
Jimbo Kuu la Mwanza lilipata hadhi ya kuwa Jimbo Kuu mwezi Februari 1988 wakati Askofu Anthony Mayala ambaye alikuwa Askofu wa jimbo la Musoma tangu mwaka 1979 aliposimikwa kuliongoza. Kusimikwa kwake kulienda sambamba na kustaafu mwaka 1987 kwa yule aliyekuwa Askofu wa Jimbo la Mwanza, Mhashamu Askofu Renatus Butibubage.
Jimbo Kuu la Mwanza linajumuisha majimbo yafuatayo: -
Jimbo Kuu la Mwanza
Jimbo la Bunda
Jimbo la Musoma
Jimbo la Bukoba
Jimbo la Geita
Jimbo la Rulenge
Jimbo la Kayanga