Parokia teule ya Bwiru ilianza kama kigango mnamo mwaka 1995, kikiwa chini ya Parokia ya Familia Takatifu Pasiansi. Katika chimbuko hili, ni Padre Bromius ambaye katika utume wake alipata kuasisi kigango hiki kwa wakati ule. Aidha, ni katika kazi zake za kitume ambapo miaka hiyo vigango vya Nyang’wilolelwa na Pasiansi kwa nyakati tofauti viliasisiwa. Katika kuimarika na kukua kwa imani kigango cha Bwiru, kilirasimishwa na kufunguliwa/kuwekewa jiwe la msingi na Hayati Askofu Mkuu Antony Mayala wa Jimbo kuu la Mwanza mnamo tarehe 12/ 01/2002. Aidha, tarehe 28/05/2018, Kigango kilipandishwa hadhi na kuwa Parokia teule na Askofu Mkuu Yuda Thadei Ruwa’ichi wa Jimbo kuu Mwanza (wakati huo).

 

MAPADRE WALIOWAHI KUHUDUMU

Katika historia, kanisa kwanza linawashukuru mapadre wote waliowahi kutoa huduma za kiroho. Wamechangia kulikuza na kuimarisha imani kwa waamini. Padre Bromius, Janusz, Segayamu, Julius, Patrick, John Baptist, Antony Gill, Patrick Machayi, Joseph Chege, na kwa sasa Parokia Teule ikihudumiwa na Pd. Josephat Nzioka (Paroko), Pd. Jeremiah Bitiong na Pd. Chewe Mweshi (maparoko wasaidizi); na wengine wote ambao hawajatajwa kwa namna moja au nyingine na kwa nyakati tofauti katika kutoa huduma. Mwenyezi Mungu awabariki sana kwa utume wao.

 

VIONGOZI HALMASHAURI WALEI WAANZILISHI

Ndugu Originos Lopa, Respicius Bishubo, Felichismi Mwijage, mzee Kirumo; kwa nyakati tofauti wameongoza kigango hiki. Mpaka kigango kupata hadhi ya kuwa Parokia Teule, viongozi hawa wamefanya kazi ya utume na kufanikiwa kuzaa kigango cha Mt. Antony wa Padua – Kitangiri, na sasa Parokia teule ikiwa na Halmashauri ya walei na Joseph Kachwele (M/kiti), Jires C. Damian (makamu M/kiti), Esther Bundala - Katibu, Fidelis Rwiza-Katibu msaidizi na Winfrida Mutta-M/hazina. Kanisa linawashukuru sana viongozi wote waliotangulia na kuonyesha njia katika kuyatakatifuza malimwengu. Mwenyezi Mungu awabariki sana.

 

JUMUIYA

Wakati kigango kinaasisiwa kilikuwa na jumla ya Jumuiya mbili (2) tu; Mt. Petro na Mt. Antony wa Padua. Mungu ni mwema, mpaka leo Parokia teule inazinduliwa ziko jumla ya Jumuiya kumi na tano (15) na vigango viwili (2).

 

MAENDELEO YA KANISA

Parokia yetu teule imepiga hatua kadhaa za maendeleo. Ni msingi pekee kuwa huduma mbalimbali za Jumuiya, ubatizo, kipaimara, ndoa, misa za katikati ya juma na kila juma na huduma zote za kanisa; ni maendeleo ambayo yamepelekea leo kuwa na hadhi rasmi ya kuzinduliwa kuwa parokia. Aidha, kutoka kusali darasani, kukalia madawati, tofali na sasa kuwa kanisa rasmi ni hatua. Hata hivyo, ununuzi wa kiwanja (square metre 17,400) cha kujenga kanisa la Parokia; ni hatua nyingine ya maendeleo na leo kupewa hadhi hii ya kuwa Parokia kamili..

 

 

UPATIKANAJI WA KIWANJA CHA KANISA

Tunawashukuru baadhi ya ndugu zetu mzee Kizwalo, Mama Mati na mzee Sabuni ambao kwa moyo wa dhati walikubali kutuachia kiwanja hiki, kwa fidia kidogo ambayo walilipwa. Tunawashukuru sana pia; mama Amina Masenza (mkuu wa wilaya wakati huo), m/kiti serikali ya mtaa - mama Kingu, Afisa ardhi wilaya Ilemela (wakati huo), mama Diana Maijo, mama Sungura, Moshi Mstafa, mama Gwanchele wakishirikiana na Respicius Bishubo, Andrew Bundala, Remi Ndesanjo na Victor Kiruma; kwa namna walivyofanikisha katika upatikanaji wa eneo / kiwanja hiki.

 

SHUKRANI

Tunakushukuru sana Baba Askofu Mkuu, Renatus Nkwande, kwa kuridhia leo hii na kuipandisha hadhi ya kuwa Parokia kamili. Mungu akubariki sana katika utume wako. Akupe afya njema ya akili na mwili katika majukumu yako ya kila siku.

 

MWISHO

Tunawashukuru sana, tena sana kwa dhati kabisa walezi wetu Parokia ya Familia Takatifu – Pasiansi. Walikubali kuwa wazazi, na kweli wametufunda katika malezi mema, mpaka leo kuwa Parokia ni kwa sababu ya mapenzi na utashi mwema walio nao katika kutulea na kuhakikisha misingi ya kiimani tunaishi na kuimarika kwa waamini wa Bwiru. Wametusaidia katika mengi, tunasema ahsanteni sana Pasiansi.