Idara hiyo ilipata nguvu zaidi ya kiutendaji kutokana na tangazo la Serikali Januari 1989 kuwa Mashirika ya dini yajiingize kikamilifu katika miradi ya kielimu.

Jimbo Kuu la Mwanza linatoa mchango mkubwa katika kuwaendeleza watu kielimu kutokana na shule mbalimbali zilizomo jimboni.

Malengo ya Idara ya Elimu:

1.    Kufufua uanzishaji wa shule za sekondari kwa kusimamia maendeleo ya wanafunzi katika taaluma na maadili.

2.    Kuhimiza uanzishaji wa elimu ya ufundi stadi katika kila parokia katika jitihada za kupunguza matatizo ya kijamii na kiuchumi wanayokumbana nayo wanafunzi wamalizao Elimu ya Msingi, na ambao hawafanikiwi kuendelea na Elimu ya Sekondari au Ualimu.

Kamati ya Elimu ya Jimbo Kuu

Idara inayo kamati ya elimu ambayo hukaa mara nne kwa mwaka kujadili ripoti zihusuzo fedha za shule na utawala, pamoja na matatizo mengine mbalimbali yanayohusu elimu. Kamati hii hutafsiri na kuweka katika vitendo taswira na utume wa Jimbo Kuu kuhusu elimu.

Dira ya kiuchungaji

Muundo wa Kamati ya Elimu unadhihirisha hali ya kiuchungaji. Licha ya zile seminari mbili (ya Mt. Mary, Nyegezi na ya Mt. Yosefu, Mwanza) shule nyingine zina sheria za shule zenye lengo la kumwendeleza mwanafunzi mzima. Ubora wa taaluma na maadili unatiliwa mkazo wakati wote, upotofu unoojitokeza hushughulikiwa bila kuchelewa. Ipo sala ya pamoja, ambayo si ya madhehebu yoyote, na inayoweza kusaliwa na wanafunzi wote katika Sekondari zote za Jimbo Kuu.

Mafungo na mazoezi ya kiroho hupangwa mara kwa mara, yakiwahusisha wanafunzi na walimu katoliki, yajenge tabia njema za kiroho na maadili katika washiriki.

Uongozi

Idara ipo chini ya uongozi kama ifuatavyo:

Mkurugenzi: Pd.Bernadin Mtula

Katibu Mtendaji: Mwl. Renatus Malimo