• archmwanza@gmail.com
  • +255 769 523 036

Kanisa Kuu Jipya Jimbo la mwanza


KUHUSU KANISA KUU JIPYA (CATHEDRAL) LA JIMBO KUU LA MWANZA

Wazo la kujenga Kanisa Kuu Jipya ni la siku nyingi sana tangu zama za Askofu wa Kwanza wa Jimbo la Mwanza Mhashamu Joseph Blomjous aliyeliongoza Jimbo kuanzia mwaka 1953-1965. Askofu Blomjous alichora mchoro wa kwanza ambapo alitaka lifanane na kanisa la Buhingo na Bujora. Mchoro huo bado upo mpaka leo. Askofu Mayala aliuboresha mchoro wa kwanza (wachoraji walitoka Baraza la Maskofu Tanzania kule Dar). Baadaye ndugu Tenga na wasaidizi wake waliuboresha zaidi mchoro na kupata mchoro wa kanisa la sasa tunaloliona. Mchakato wa ujenzi wa Kanisa Kuu jipya umechukua takribani miaka 60. Mchakato huu uliendelea kupata msukumo wakati wa uongozi wa hayati Askofu Mkuu Anthony Petro Mayala. Askofu Mkuu Anthony Mayala alipenda Kanisa Kuu lijengwe katika kilima cha Kawekamo ili kuenzi ujio wa Baba Mtakatifu Yohane Paulo II katika eneo hilo la Kawekamo. Mwaka 2003 Hayati Askofu Mkuu Anthony Petro Mayala aliunda kamati ya uhamasishaji wa ujenzi wa Kanisa Kuu chini ya uongozi wa Jaji mstaafu Mathias Nchalla. Mchakato ulichukua muda mrefu sana kwa kuwa  Askofu Mayala alitaka watu wapewe kwanza wazo, walipokee, walione ni lao na kisha kulitekeleza.

Hatua za awali kuelekea ujenzi wa Kanisa Kuu zilianza kufanyika zikiwemo kuandaa michoro, kutathmini gharama za ujenzi na upatikanaji wa fedha ili kufanikisha ujenzi huo. Kamati ya ujenzi wa Kanisa Kuu iliandaa harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa Kuu Novemba 22, 2003. Mwaka 2004 moto wa ujenzi wa Kanisa Kuu ulipoa baada ya fedha iliyopatikana kutokana na harambee kumalizika kwa malipo ya awali kwa wasanifu na kwa shughuli za awali zilizokuwa zimefanyika (kufyatua tofali, kupasua mawe na kujenga bohari katika eneo la ujenzi). Miaka iliyofuata uhamasishaji wa michango ya ujenzi uliendelea kufanyika katika ngazi ya parokia. Mwaka 2009 Askofu Mkuu Anthony Petro Mayala alikusudia kusaini rasmi mkataba na kampuni ya ujenzi ili kuanza rasmi mradi wa ujenzi wa Kanisa Kuu. Tarehe 17/08/2009 ndiyo ilikuwa siku ya mkandarasi kukutana na Askofu Mkuu Mayala lakini mkandarasi hakuweza kufika. Kufuatia kifo cha ghafla cha Askofu Mkuu Anthony Petro Mayala mnamo Agosti 19, 2009 (siku mbili tu tangu walipopanga kukutana na mkandarasi), shughuli nzima ya ujenzi wa Kanisa Kuu ilisimama. Padre Renatus Nkwande, akiwa Msimamizi wa Jimbo, aliona siyo busara kuendelea na ujenzi wa Kanisa Kuu ilihali Jimbo lipo wazi.

Januari 9, 2011 Askofu Mkuu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi alisimikwa kuliongoza Jimbo Kuu la Mwanza. Baada ya kusimikwa kwa askofu Ruwa’ichi harakati za ujenzi wa Kanisa Kuu zilianza tena kupewa msukumo mpya. Katika hotuba yake ya kusimikwa alisisitiza kuendeleza mikakati ya mtangulizi wake hasa ujenzi wa Kanisa Kuu. Baba Askofu Mkuu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi aliunda kamati mpya ya ujenzi na alianza rasmi mfululizo wa vikao vya kamati hiyo tarehe 29/10/2011. Juhudi hizo ziliendelea licha ya changamoto mbalimbali kama vile upatikanaji wa fedha, maboresho ya mchoro wa Kanisa Kuu (Cathedral), ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wasimamizi na wakandarasi waliochaguliwa na mengineyo. Uzinduzi wa ujenzi huo ulifanywa rasmi kwa Misa Takatifu tarehe 16/10/2012 Kawekamo. Baada ya kufanya mabadiliko kadhaa katika mchoro wa Kanisa Kuu, sasa Kanisa Kuu jipya litakuwa na uwezo wa kuchukua waamini kati ya 5000 na 6000 waliokaa, litakuwa na ofisi 4 ikiwemo ya Baba Askofu Mkuu, litakuwa na kanisa dogo moja, litakuwa na kumbi mbili (2) za mikutano zenye uwezo wa kubeba watu 100 kila moja, litakuwa na makaburi 8 kwa ajili ya kuzikia Maaskofu, mbele ya kanisa kutakuwa na minara miwili yenye urefu wa ghorofa saba. Gharama zinazokadiriwa ili kukamilisha ujenzi wa Kanisa Kuu ni 6,600,000,000 (Bilioni sita na milioni mia sita).