• archmwanza@gmail.com
  • +255 769 523 036

Historia Fupi Ya Parokia Ya Kishiri

Parish Details

HISTORIA  FUPI  YA  PAROKIA  YA

MT. LUKA  MWINJILI -  KISHIRI


Parokia ya Kishili (neno Kishili linatokana na neno la Kisukuma “shiili” lenye maana ya “kunde” - eneo la Kishili lilikuwa ni eneo maarufu kwa kilimo cha kunde) ina chimbuko lake katika Parokia ya Bujora. Mwaka 1975 kundi la waamini likiongozwa na ndugu Thobias Mayengela Ndumi (wakiwa waamini wa Bujora) walianza kusalia nyumbani kwa muumini mmoja eneo la Kishili kutokana na umbali wa kwenda Parokiani Bujora. Baadaye iliundwa kwaya ambayo ilipita nyumba kwa nyumba kuhamasisha waamini kujiunga na kusali pamoja. Kwaya hii iliwavutia hata wapagani na hivyo idadi ya waamini na waliokuwa na nia ya kubatizwa iliongezeka. Kwaya iliyokuwa imeundwa ilizidi kuwa kivutio cha wengi kujiunga na ukatoliki maana ilikuwa ikishiriki hata kwenye matukio ya kijamii kama vile misiba. Mwaka 1977 ilibidi waombe chumba kimoja cha darasa katika shule ya msingi Kishili ili wakitumie kwa ibada na Misa siku za Jumapili.


Mnamo mwaka 1978 serikali ya kijiji cha Kishili iliamua kutenga maeneo kwa ajili ya Taasisi mbalimbali ambapo Kanisa Katoliki lilitengewa eneo lilipo sasa kanisa la Parokia ya Kishili. Awali eneo hilo lilimilikiwa na ndugu Issa Nhigula. Hata baada ya kupata eneo hilo bado waamini waliendelea kusalia katika chumba cha darasa mpaka mwaka 1993 walipojenga kigango chini ya uongozi wa hayati Padre Alexander Mugonya aliyekuwa Paroko wa Bujora. Baadaye ilianzishwa Parokia ya Igoma ikimegwa kutoka Parokia ya Bujora na hivyo kigango cha Kishili kikawa moja ya vigango vya Parokia ya Mt. Josephina Bakhita Igoma chini ya Paroko Padre Andreas Msonge.


Mnamo mwaka 2004 waamini wa kigango cha Kishili walipata wazo la kujenga kanisa kubwa zaidi la kigango maana kanisa la awali lilikuwa dogo kutokana na idadi ya waamini kuongezeka siku kwa siku. Wazo hilo lilianza kuwekwa katika uhalisia mwaka 2007 pale shughuli ya ujenzi wa kanisa kubwa ilipoanza kwa kuchimba mashimo na kusimika nguzo za kanisa. Ujenzi huu umeendelea katika hatua mbalimbali hadi sasa linapoendelea kupendeza. Mnamo tarehe 20/01/2017 kigango cha Kishili kilitangazwa rasmi kuwa Parokia Teule na Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi kikiendelea kuwa chini ya usimamizi wa Padre Kessy Baltazary aliyekuwa Paroko wa Parokia ya Igoma. Baadaye Parokia Teule ya Kishili iliwekwa chini ya usimamizi wa Padre Richard Makungu hadi mnamo 18/10/2019 ambapo ilipandishwa hadhi ya kuwa Parokia kamili na kuzinduliwa na Askofu Mkuu Renatus Nkwande na kumsimika Padre Richard Petro Mkungu kuwa Paroko wa kwanza wa Parokia ya Mt. Luka Mwinjili Kishili. Wakati inazinduliwa rasmi kuwa parokia, Parokia ya Kishili ilikuwa na vigango vinne tu vya Bukaga, Kanindo, Fumagila na kigango mama cha Kishili. Kwa sasa imeongeza vigango vingine vitatu vya Ndofe, Ng’wanghalanga na Kanenwa. Hata hivyo tayari kigango cha Bukaga kimeshatangazwa kuwa Parokia Teule. Kanisa la Parokia ya Kishiri lilitabarukiwa mnamo 22/10/2022.



 

 

Parish Images

Parish Videos