• archmwanza@gmail.com
  • +255 769 523 036

Parokia ya Bugando

Parish Details

Mji wa Mwanza ulianza polepole kama bandari kiunganishi cha kimataila cha biashara baina ya Uganda na Kenya kwa njia ya meli na reli ya Mombasa. Kutoka kijiji cha wakulima na wavuvi ghafla ikawa ngome ya maaskari, makao ya serikali, ofisi ya Posta, Ushuru wa forodha na Kituo cha polisi. Wahindi wakaanza kufungua maduka, watu wengi wakafika Mwanza kufanya kazi za vibarua ili waweze kupata pesa za kulipa kodi ya kichwa, madeni na mahari. Wengine walitafuta ajira za ukarani, wafanyakazi wa ndani kwa wahindi, wazungu na wagoa.

 Mizigo ya wamisionari kutokea ng'ambo kuelekea Uganda, Kongo na Unyanyembe ilipitia na kupokelewa Mwanza. Kila mara afisa wa forodha alimuhitaji Padre kutoka Bukumbi kutafasiri maelezo ya mizigo yaliyoandikwa kwa Iugha ya kifaransa kabla ya mizigo haijapokelewa na wahusika. Kutokana na safari ya nenda rudi iliamriwa kuanzisha kituo cha kushughulikia mizigo. Kituo hicho kiliwekwa juu ya kilima cha Bugando, nje ya mji wakati huo. Hivyo ikanunuliwa nyumba ya zamani yenye vyumba vitatu, kikubwa kikafanywa Kikanisa, na vile viwili wakakaa wamisionari wawili. Ufinyu wa nafasi katika nyumba hiyo ulidhihirisha kwamba wamisionari waliopitia Mwanza kutokea Ulaya ilibidi walale kwenye mahema. Jiwe la msingi wa Kanisa liliwekwa tarehe 10, Machi, 1907 na Askofu Hirth akidhamiria Parokia itawekwa chini ya ulinzi na usimamizi wa Mama yetu wa Rozari Takatifu, lakini mfadhili aliyetoa pesa ya kununulia nyumba pale Bugando alikuwa anakaa Kolon Ujeremani ambapo katika Kanisa la Kolon kumehifadhiwa masalia ya mamajusi. Akaomba kanisa litakalojengwa liwekwe chini ya uangalizi wa Mamajusi. Hivyo parokia na baadaye Kanisa Kuu (Cathedrali) ikawa na jina hilo la Epifania. Hata hivyo jengo la mwanzo halikudumu lilishambuliwa na mchwa na paa likaanguka. Bruda Marie alisimamia ujenzi wa majengo mapya mawili kwa kutumia matofali ya kuchoma juu ya msingi imara wa mawe.

Wakati huo vibarua katika mji wa Mwanza hawakuwa wengi, na malipo yao yalikuwa aghali, rupia saba kwa mwezi. Mavuno mwaka huo hayakuwa mazuri, wasukuma wengi walikuwa wamekwenda kufanya kibarua katika ujenzi wa reli kutoka Dar es Salaam kuelekea Morogoro. Malipo yalikuwa juu zaidi kwani walilipwa rupia kumi na sita kwa mwezi, sawa na Tsh.8,000 na walipewa chakula cha kutosha. Kila mara alfajiri kulisikika mwaliko wa sala kutoka misikiti sita ambayo tayari ilikuwepo mjini Mwanza. Polisi na maaskari walikuwa watu waliotoka pwani ambako Uisilam ulikuwa umestawi. Hivyo sherehe za Kiislam zilikuwa pia siku za mapumziko Kitaifa. Mazishi ya kiislam yalikusanya umati mkubwa na kuwa kivutio kwa wenyeji. Wengi waliobahatika kupata ajira mjini Mwanza walijiunga na dini ya Kiislam. Muumini mmoja alitoa taarifa kwamba, "Tulikuja kundi la wakristu kumi kutoka Uganda, wenzangu wote wamebadili dini na kuwa waislam". Hata siyo wote walioajiriwa walifuata ushawishi wao.

Katika kikanisa cha Bugando takribani waamini hamsini walishiriki Misa ya Jumapili, wengi wao wakiwa wale waliotokea Bukumbi, Ukerewe, Ushirombo na Uganda. Palikuwa pia na idadi ya familia za Wagoa. Hivyo licha ya mapadre kushughulika na shughuli za forodha ilibidi watolee muda pia kwa ajili ya kuwahudumia kiroho jamii ya waamini waliokuwa wanaiishi Mwanza. Mafundisho ya wakatekumeni yalitolewa mara tatu kwa juma. Baada ya miaka minne idadi ya waamini mjini Mwanza iliongezeka mara tatu. Kanisa lilipanuliwa ili kukidhi ibada ya Jumapili, hata siku za juma mahudhurio yaliongezeka kufikia idadi ya watu arobaini kila siku.

Hapo awali Mapadre walipopita mjini walikuwa wanaitwa wafaransa, lakini baadaye wakatambulika kwa kuitwa Mapadre. Padre Jongerius alianzisha shule iliyovutia wanafunzi sitini licha ya ushindani mkubwa uliokuwepo kati ya kanisa na serikali ambayo ilileta mwalimu kutoka Ujerumani. Shule ya wasichana ilianzishwa pia na kusimamiwa na mwanamama mmoja aliyeitwa Juliana. Mapadre walitarajia kwa baadaye masista wa Kiafrika kuja kubeba jukumu hilo.

Utume ulipanuka hadi vijiji vilivyozunguka mji, vigango viwili vilianzishwa, kimoja pale Nyegezi mbacho kilijumuisha pia na shule iliyosimamiwa na Katekista. Ndani ya miaka mitatu tayari kulikuwa na wakatekumeni mia tatu. Kijana mmoja kwa jina Cajetan aliomba mdali kama msaada kwa dada yake, alieleza, "Dada yangu kila ahudhuriapo mafundisho huchapwa na baba, hulazimishwa kuolewa na mpagani, nikimpelekea mdali huu akauvaa baba ataogopa kumpiga na mpagani anayetaka kumuoa atakata tamaa na kumwacha huru." Tayari Cajetan aliishafanikiwa kuwaleta wadogo zake wawili na kufuata mafundisho licha ya katazo la baba yao.

Parish Images

Parish Videos