• archmwanza@gmail.com
  • +255 769 523 036

Parokia ya Kahama

Parish Details

HISTORIA YA PAROKIA YA

MT. THERESIA WA MTOTO YESU -  KAHAMA

 

Kigango cha Mt. Theresia wa Mtoto Yesu – Kahama, kilianzishwa mnamo mwaka 1974, Wakati huo walikuwa wanasali nyumbani kwa Judith Kapesa, ambae alihudumu kama katekista kwa wakati huo. Mwaka 1983, walihamia katika maeneo ya shule ya msingi Kahama, wakiwa chini ya katekista TRYPHONE KABABASHE NG’HOLONGO, wakiwa chini ya Parokia ya Mt. JUSTINE – BUJORA. Baada ya kufariki katekista TRYPHONE, Waliendelea kusali wakiwa na katekista CLEMENT LUMU MAYALA.

Mnamo mwaka 1985 walianza ujenzi wa Kanisa katika eneo walilopewa na serikali ya kijiji chini ya uongozi wa Andrea Mang’weng’ula (mwenyekiti wa kijiji) na Zabron Kalimbia (kamati ya ugawaji ardhi), wakati huo walikuwa chini ya katekista Venance Makelele. Walianza ujenzi wa kanisa la tope na kuezeka kwa nyasi kwa kutumia nguvu za waumini. Na mwaka 1994 walipata ufadhili wa mabati hamsini (50)  kutoka kwa Padre KALORI wa parokia ya Kawekamo, na wakati huo walikuwa chini ya usimamizi wa katekista Joseph Ludaila Nyanda.

 

Mwaka 2005 kigango cha Mt. Theresia wa Mtoto Yesu kilikabidhiwa chini ya usimamizi wa parokia ya Mt. Josephina Bakhita – Igoma chini ya usimamizi wa Padre ANDREA. Wakati huo kigango kilikuwa na jumuiya nne (4), ambazo ni jumuiya MT. THERESIA, VERONICA, MARIA NA YOSEPH, na wakati huo kigango cha Kahama kilitumika kama senta ya vigango vitatu ambavyo ni Igogwe, Nyamadoke na Kahama. Mwaka 2014 jumuiya ya Mt. Maria iligawanywa na kupata jumuiya ya Mt. Petro ambayo baadae ilianzisha  kigango cha Isela.

 

Tarehe 01/01/2018, kigango kiliwekwa chini ya usimamizi wa parokia ya Bikira Maria Mama wa Mungu – Buswelu, kikiwa na jumuiya ndogo ndogo kumi na saba (17). Wakati huo kigango kilikuwa chini ya katekista Christopher Swalala ambaye kwa sasa ni marehemu. Tarehe 26/09/2020 kigango cha Mt. Theresia wa Mtoto Yesu – Kahama kilitangazwa kuwa Parokia Teule na Mhashamu Baba Askofu Mkuu Renatus Leonard Nkwande, chini ya usimamizi wa Padre Faustine Yohane Bagwa hadi leo tarehe 29/10/2022, Parokia Teule Kahama ina vigango vitatu ambavyo ni kigango cha Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu – Kahama chenye jumuiya ishirini (20) na mitaa tisa (9), kigango cha Mtakatifu Petro Mtume- Ilalila chenye jumuiya sita (6) na kigango cha Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu – Igogwe chenye jumuiya tano (5). Hivyo Parokia Teule ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu – Kahama ina jumla ya vigango vitatu (3), mitaa tisa (9) na jumuiya thelathini na moja (31).

 

Parish Images

Parish Videos