Parish Details
HISTORIA YA PAROKIA YA BUHINGO
Parokia ya Moyo Mtakatifu
wa Yesu Buhingo inapatikana katika wilaya ya Misungwi umbali wa kilometa 80
toka Mwanza mjini. Ni moja kati ya Parokia 61 zinazounda Jimbo Kuu la Mwanza na
ndiyo Parokia kubwa kuliko zote katika Jimbo Kuu la Mwanza ikiwa na vigango 46,
Parokia Teule 3 za Misasi, Ibinza na Kasololo na waamini Wakatoliki takribani
25,000. Kwa miaka 100 imehudumiwa na mapadre mbalimbali, wakiwemo Mapadre wa
Mashirika hasa Wamisionari wa Afrika (White Fathers) pamoja na Mapadre
Wazalendo wa kwanza Tanzania wakiwemo Wilbald Mupapi, Angelo Mwilabure na
Celestine Kipanda “Kasisi”. Mupapi na Kipanda walihudumu Buhingo kwa takribani
miaka 16 kwa nyakati tofauti. Buhingo imewahi kuhudumiwa pia na hayati Askofu
Renatus Butibubage wa Mwanza! Buhingo kumenoga! Ikumbukwe kwamba Parokia ya
Buhingo inachota historia yake toka Parokia ya Bukumbi, Parokia ya kwanza
kabisa kuanzishwa katika Jimbo Kuu la Mwanza. Mapadre Wamisionari waliwasili
eneo la Bukumbi mwaka 1883 wakitokea Uganda baada ya kupata upinzani mkubwa
toka kwa Waprotestanti na kutoka kwa Kabaka mfalme wa Buganda. Walipowasili
Bukumbi walipokelewa na Chifu Kiganga wa Kigongo na kupewa eneo la kuanzisha
Misioni Bukumbi. Na hivyo Bukumbi ikawa parokia ya kwanza ya Jimbo Kuu la
Mwanza na huduma mbalimbali za kiroho zikaanza mara moja. Baadaye wamisionari
hao waliona uhitaji wa kupanua huduma za kiroho maeneo mbalimbali na hivyo
mwaka 1902 Mapadre Wamisionari waliokuwa wakihudumia Parokia ya Bukumbi
walifungua vigango mbalimbali katika eneo la kusini mwa Bukumbi, yaani Buhingo
ya wakati huo. Vigango vilivyofunguliwa katika eneo la Buhingo ya nyakati hizo
ni Igudija (Bugisha), Isesa (Gukuma), Igenge, Nyabuhele (Mbalika) na Sasi
(Ng’wasagela).
Ombi la Helena Majenga wa kigango cha Isesa
(Gukuma)
Baada ya kufunguliwa kwa kigango cha Isesa
(Gukuma), mwaka 1920 binti mdogo kutoka kigango hicho aitwaye Ng’wana Majenga
alithubutu kwenda Bukumbi kuomba abatizwe. Alifundishwa mafundisho ya dini
katoliki kwa miaka miwili. Huko Bukumbi Ng’wana Majenga alipata bahati ya
kukutana na binti mwingine kutoka Kasololo aliyeitwa Bibiana Fundi akiwa na
umri wa miaka 16. Ng’wana Majenga alibatizwa na kupewa jina la Helena. Helena
Majenga aliporudi Gukuma (Isesa, sasa kigango cha Parokia ya Mbalika) akitokea
Bukumbi aliwavuta wasichana wengine wawili katika imani. Wasichana hao wawili
walibatizwa na kupewa majina ya Fransiska Shinaga na Margareth Izengo. Helena
Majenga na wenzake walizoea kwenda kila mwezi Bukumbi kwa mtumbwi katika ziwa
Victoria ili kupokea Ekaristi Takatifu. Katika safari yao kuelekea Bukumbi
walikumbana mara kwa mara na hatari, hasa ziwani (Ziwa Victoria) maana
walipaswa kupanda mtumbwi toka Gukuma (Mbalika) hadi Bukumbi: hatari ya mamba
na mitumbwi kupinduka. Lakini hata baada ya kutoka ziwani iliwapasa kutembea
kwa miguu na njiani kulikuwa na tishio la wanyama wakali. Hatari hizi ndizo
zilizopelekea Helena Majenga na wenzake kumwandikia Padre Vekemans (maarufu
kama Venge) aliyekuwa akihudumu Bukumbi ujumbe maalum: “Afadhali, njoni kwetu
Bulima kwa Mtemi Nkondo Lunyalula; mwombeni ploti, mkajenge Misioni…” Padre
Vekemans hakusita na mwaka 1921 alifika kwa Mtemi Nkondo kuomba eneo ambapo
alipewa ploti katika eneo la Nyabuhele mwendo wa kilometa 3 toka Mbalika. Hata
hivyo baadaye mahusiano kati ya mtemi Nkondo na Padre Vekemans yaliingia dosari
baada ya mtemi Nkondo kufikiri kuwa Mapadre watabadili mawazo ya watoto wake na
hivyo kuwa na misimamo tofauti ya kumpinga. Hali hii ilimfanya Padre Vekemans
kwenda kumwonya mtemi na “kuiangusha kofia ya mtemi” kwa ukali. Kutokana na
mgogoro huu padre Vekemans aliamua kuhamia Kashishi baada ya kupokelewa kwa
furaha na mtemi Mpuya bin Kwangu wa Busongo. Wamisionari walifanikiwa kuanzisha
“bush school” eneo la Kashishi.
Mwaka 1922 Mapadre wa Bukumbi waliitambua Kashishi kama Senta na kiunganishi kati ya Buhungukila (kusini), Nera (Mashariki) na Bulima (Kaskazini). Huu ulikuwa ni mwanzo mzuri wa uenezaji wa Injili katika maeneo yaliyozunguka Buhingo. Kati ya mwaka 1922 hadi 1923 Padre Michel Gass raia wa ufaransa aliyekuwa akihudumu Parokia ya Bukumbi alijaribu kuanza ujenzi wa kanisa la kwanza la udongo pamoja na nyumba ya muda ya mapadre katika eneo la Kashishi. Nyuma ilikuwa na vyumba viwili tu: chumba cha chakula na chumba kidogo cha kulala watu watatu. Mapadre walilala kwa kujibanabana sana na wengine walilalia majani. Baadaye waliwasili kwa baiskeli kutokea Bukumbi Mapadre wawili wahaya Padre Wilbald Mupapi (alikuwa Paroko) na Trifoni Rwechungura. Hawa waliendeleza kazi ya ujenzi hapo Kashishi. Hata hivyo kazi ya ujenzi haikuwa rahisi maana vibarua walikuwa haba, baadhi ya wenyeji walikataa kazi ya kuleta mawe, miti na majani na hata mafundi hawakupatikana kirahisi. Hata hivyo penye nia pana njia kwani Oktoba 21, 1923 alifika Padre Vekemans (Venge) kubariki kanisa lililojengwa. Ilikuwa siku ya furaha kubwa maana sherehe ilidumu kwa siku mbili mfululizo ambapo watu walikula, kunywa na kusaza huku miili ikiburudishwa kwa ngoma za asili. Tarehe 19 Aprili 1924 walibatizwa waamini wa kwanza katika Parokia ya Kashishi. Mnamo 27 Desemba 1924 Askofu Joseph Sweens kutoka Bukoba alifika kukagua misheni ya Kashishi na hata kuazima gari kwa ajili ya kusomba mawe kufanikisha kazi za ujenzi zilizokuwa zinaendelea hapo Kashishi. Askofu Sweens alikuwa akitumia usafiri wa punda. Majanga ya mara kwa mara yalazimu Parokia kuhamishiwa Buhingo ilipo sasa: Mnamo mwaka 1928 kulitokea mafuriko makubwa sana ya mvua eneo la Kashishi na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa katika misheni ya Kashishi: nyumba za mapadre ziliharibika, mikaratusi ilianguka, paa la kanisa likang’olewa na kupeperushwa na vitu vitakatifu vikadhurika sana. Hali hii iliwafanya mapadre kuhamia shuleni hapo Kashishi kwa huzuni kubwa. Majanga ya mara kwa mara yaliyosababishwa na mvua yaliendelea kuwa changamoto kubwa maana eneo la Kashishi lilikuwa mbugani. Hali hii ilimfanya Askofu Sweens awahurumie sana mapadre na kuamua Parokia ya Kashishi ihamie juu ya kilima kidogo cha BUHINGO ambapo palikuwa pakavu zaidi. Neno “Buhingo” siyo neno la Kisukuma kwa asili bali ni neno la kabila la Balongo maana katika eneo hilo walikaribishwa watu wa kabila la Kilongo ambao walijishughulisha na uhunzi wa majembe “magembe” na pia walikuwa mafundi wa kuyeyusha mawe ili watengeneze namna ya vidonge vya chuma vilivyokuwa na umbo kama mpira wa tenesi. Kidonge kiliitwa “kihingo.” Kwa kuwa kidonge cha chuma kiliitwa kihingo, wasukuma wakaanza kuwaita watengenezaji wa kidonge hicho Bahingo. Baada ya muda sehemu walipofanyia kazi “Bahingo” pakaanza kuitwa Buhingo.
Baada
ya maamuzi ya Askofu ya kuhamisha Parokia kutoka Kashishi kwenda Buhingo (ilipo
sasa parokia), mnamo tarehe 06/06/1933 Askofu Sweens alifika Buhingo akiwa na
Brother Beatus aliyekuwa
mtaalamu wa ujenzi (alijenga pia Nyegezi Seminari) na kuanza upimaji wa nyumba
ya Misioni Buhingo na kusaidiana na waamini kufyeka eneo na kufukuza wanyama
wakali. Waliamua kujenga Kanisa la msonge kwa kufuata muundo wa nyumba za
kisukuma za wakati huo. Ndivyo ilivyozaliwa misioni ya Buhingo. Na baadaye
ikajengwa shule. Kwa sasa Parokia ya Buhingo ina vigango 46 na Parokia Teule 3
za Misasi, Ibinza na Kasololo. Kwa takribani miaka 100 Parokia ya Buhingo
imepiga hatua kubwa za kimaendeleo zikiwemo ujenzi wa makanisa imara na ya
kudumu katika vigango, ujenzi wa nyumba za mapadre katika Parokia teule,
maboresho ya nyumba kubwa ya mapadre iliyojengwa na wamisionari pamoja na
ujenzi wa nyumba mpya ya Mapadre Buhingo na Misasi. Kwa miaka 100 Parokia ya Buhingo
imetoa Mapadre wazawa watatu: Padre Alex Kitwala, Padre Moses Mapela na Padre
William Ndhone. Parokia ya Buhingo inayo pia waseminari wakubwa waliopo katika
majiundo ya wito wa upadre na inayo pia waseminari wadogo katika seminari za
Nyegezi, Makoko, Shanwa na Sengerema. Hata hivyo licha ya mafanikio haya bado
katika maeneo ya Buhingo kuna mila, mawazo na desturi potofu kama vile kuamini
kuwa watoto wanaozaliwa mapacha huleta laana katika jamii, wakazi kuchangishana
pesa ili kumleta mtu wa kuleta mvua (abagemi ba mbula) nyakati za ukame, mauaji
ya wanawake kwa imani ya kupata utajiri. Pamoja na changamoto hizi pia ukubwa
wa parokia na wingi wa vigango vimekuwa vikwazo vya ufanisi wa kichungaji.
Katika maandalizi ya kilele cha Jubilei zaidi ya waamini 900 wamebatizwa, zaidi
ya waamini 500 wamepokea Komunyo ya kwanza na jozi 10 zimefunga ndoa na katika
siku ya kilele cha Jubilei zaidi ya waamini 300 wataimarishwa kwa Sakramenti ya
Kipaimara, kubariki nyumba mpya ya mapadre inayoendelea kujengwa na kusimika
Msalaba wa Jubilei. Ijumaa Julai 21, 2023 waamini na maaskofu watakaohudhuria
watafanya maandamano toka eneo la Kashishi ilipoanza Misioni ya kwanza hadi
Parokiani Buhingo, maandamano yatakayoenzi safari ya Mapadre toka Kashishi hadi
Buhingo.